
Msimu wa ligi si wa mafanikio kwa Manchester City
baada ya klabu hiyo kushindwa kutetea taji lao la ligi kuu ya England
ambalo walitwaa msimu uliopita na pia wameshindwa kwenda mbele kwenye
michuano ya ligi ya mabingwa baada ya kutolewa kwenye hatua ya 16 bora.
Kingine ambacho huenda sio taarifa nzuri kwa Klabu ya Manchester City ni taarifa za kuondoka kwa kiungo wao kutegemewa, Yaya Toure.
Dimitri Seluk ambae ni wakala wa kiungo huyo raia wa Ivory Coast, Yaya Toure amevithibitishia
vyanzo mbalimbali vya habari hii kuwa mteja wake ana uhakika wa 90%
kuihama klabu hiyo baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Wakala huyo amefichua kuwa uhusiano wa Yaya na Manchester City
umekuwa mbovu na imefikia hatua mbaya kiasi cha mchezaji huyo kufanya
maamuzi ya kuondoka na kufikia uamuzi ambao hawezi kuubadilisha.
Itakumbukwa kuwa kiungo huyo aliingia
kwenye ugomvi ambao uliripotiwa sana kwenye vyombo vya habari mwaka jana
wakati klabu yake iliposhindwa kumfanyia hafla ya siku yake ya kuzaliwa
wakati City ilipokuwa kwenye ziara ya huko Falme Za Kiarabu ripoti ambazo baadae zilikanushwa.
Wakati hayo yakiendelea Yaya Toure kwa nyakati kadhaa amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na kocha wake wa zamani Roberto Mancini ambaye kwa sasa anaifundisha Inter Milan.
Kwa upande wa uongozi wa Man City
inasemekana kuwa klabu hiyo inajiandaa kusikiliza ofa zitakazokuja kwa
ajili ya mchezaji huyo kutokana na umri wake kusogea huku uongozi ukiwa
na mpango wa muda mrefu wa kujenga kikosi cha City kwa kuwategemea zaidi wachezaji wenye umri mdogo.

Post a Comment